Menu
 

Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
 Asasi ya Tehilah Foundation ambayo pia inamiliki Shule ya Sekondari ya Vanessa iliyoko Isyesye Jijini Mbeya imetoa msaada wa fedha taslimu shilingi Milion 55 kwa ajili ya watoto yatima 31.
 
Akikabidhi Msaada huo kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Vanesa Osward Mwachande, Mkurugenzi wa Asasi hiyo Shukrani Mwasanjobe alisema fedha hizo ni kwa ajili ya ada ya watoto yatima 31 wanaosoma kidato cha kwanza na kuongeza kuwa ada hiyo itawasaidia hadi kidato cha nne.
 
Alisema lengo ni kupunguza wimbi la watoto yatima mitaani kutokana na wingi wa watoto hao kuondokewa na wazazi wao kwa Ugonjwa wa Ukimwi ambapo wengi wao wamekuwa watelekezwa na ndugu baada ya wazazi wao kufariki.
 
Aidha aliiomba jamii nyingine kusaidia watoto hao upande wa michango mingine kama sare za shule na madaftari ambapo yeye amelipia ada kwa miaka mine.
 
Pia aliwasihi walezi wa watoto hao kuwahimiza kusoma na kuhudhuria masomo ili waweze kufaulu kidato cha nne na kuendelea katika masomo ya juu ambako pia ni rahisi kupata misaada kutoka kwa wasamaria wema.
 
Alisema watoto wanaonufaika na msaada huo wanatoka katika kata za Iyunga, Isanga, Isyesye, Nzovwe na Mbalizi Road zote za Jijini hapa ambao wengi wao walifauru kujiunga kidato cha kwanza katika shule za Serikali lakini hawakujiunga kutokana na ukosefu wa ada.
 
Akitoa Shukrani kwa niaba ya walezi wa watoto hao Mtendaji wa Kata ya Isanga Fideris Mwaselela alisema mchango wa mkurugenzi huyo umeisaidia Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambayo ndiyo iliyokuwa na jukumu la kuwasomesha watoto hao.
 
Aliongeza kuwa watoto hao wakifaulu vizuri ndiyo watakaokuwa wataalamu wa baadaye na kuisaidia jamii na taifa kwa ujumla katika kazi za maendeleo.
 
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii kata ya Isyesye Jiji la Mbeya Rose Kitundu alisema idara yake inamshukuru mkurugenzi huyo kwa kutatua tatizo lililokuwa likiwakabili watoto hao.
 
Alisema jukumu la kusaidia watoto hao ni la kila mtu ambapo aliongeza kuwa Mkurugenzi huyo amewaokoa katika kujiingiza kwenye vitendo visivyofaa kutokana na kuzurura mitaani.

Post a Comment

 
Top