Menu
 


Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
 MWALIMU mkuu pamoja na uongozi wa Serikali ya Kitongoji cha Iyunga kata ya Ilembo wanatuhumiwa na wananchi wao kutafuna fedha za michango ya wananchi pamoja na zilizotolewa na serikali.
 
 
Watumishi hao wa umma wanatuhumiwa kufuja fedha ambazo zilichangwa na wananchi kwa ajili ya kusakafia vyumba vya madarasa ambazo ni shilingi Milioni 1,640,000/=.
 
 
Fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu zinazodhaniwa kutafunwa na viongozi hao ni shilingi Milioni tisa(9,000,000/=).
 
 
Mwalimu anayetajwa kuhusika na skendo hiyo ni Mwalimu Ibrahimu Amosi ambaye alikuwa Mwalimu mkuu katika Shule ya msingi Hazina ya kijijini hapo ambapo kufuatia tuhuma hiyo Mwalimu huyo alihamishiwa katika shule ya Msingi Mbagala ya kata ya Ilembo.
 
 
Kwa upande wa viongozi wa Kitongoji wanaotuhumiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa bodi ya shule ya Hazina Allan Mbwiga,Mwenyekiti wa kitongoji Bonifasi Uledi, Stefano Oswadi na Christina Richard ambao pamoja na ubadhilifu huo pia hawajasoma mapato na matumizi kwa kipindi cha mwaka mzima. 
 
 
Kutokana na ubadhilifu huo Wananchi wamekatishwa tamaa na kuendelea kuchangia ujenzi wa shule hali iliyopelekea wanafunzi kurundikana katika madarasa yaliyojaa vumbi huku walimu wakikosa nyumba za kuishi.
 
 
Aidha wanafunzi hao wako hatarini kupata magonjwa mbali mbali kutokana na vyumba hivyo kujaa vumbi ambapo chumba kimoja kina wanafunzi zaidi ya 70 pia walimu ambao hulazimika kutembea zaidi ya kilomita 4 kuifuata shule hiyo.
 
 
Hata hivyo Kufuatia tuhuma hizo Katibu tawala msaidizi wa Wilaya ya Mbeya Geophrey Anania alikiri kupokea tuhuma hizo na kuongeza kuwa tayari ametuma tume kuchunguza tuhuma hizo.
 
 
Alisema tume hiyo ikimaliza kazi hiyo atatoa taarifa kama kweli wamehusika na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa watakaohusika na tuhuma hizo ambapo alisema muda wa tume hiyo ni mfupi kutokana na hali ya vyumba vya madarasa ilivyo.

Post a Comment

 
Top