Menu
 


Mamia ya wagonjwa mkoani Kigoma wamejitokeza kuonana na jopo la Madaktari bingwa kutoka hospitali ya Taifa ya Mhimbili waliopelekwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya NHIF ambao unaendesha mpango wa kuwapeleka madaktari hao mikoa mbalimbali ya pembezoni mwa Tanzania.

Mpango huo wa NHIF una lengo la kuwasaidia wanachama wake pamoja na wananchi wa kawaidia kupata huduma za wataalamu hao wakiwa maeneo yao hivyo kuepuka kufuata huduma zao jijini Dar es salaam au Mwanza.

Akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Mkoa ya Maweni mkoani Kigoma, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Ramadhan Maneno amesema kuwa kitendo cha NHIF kupeleka madaktari hao ni cha kupongezwa kwa kuwa kina lengo la kuokoa maisha ya wananchi na kupunguza gharama pia kusaidia kuboresha huduma katika maeneo husika.

Naye Naibu Mkurugenzi wa NHIF, Hamis Mdee akitoa maelezo ya awali kabla ya madaktari hao kuanza kazi rasmi, amesema kutokana na matatizo makubwa ya upatikanaji wa wataalam hasa katika mikoa ya pembezoni, mfuko umeanza utaratibu wa kuwapeleka madaktari bingwa katika mikoa hiyo na kutoa huduma na hasa za upasuaji.

Mikoa mingine inayotarajiwa kufikiwa na mpango huu ni Rukwa, Katavi na Mkoa wa Pwani.

Post a Comment

 
Top