Menu
 Leo ikiwa mwaka wa pili toka  nifanikishe kurusha chapisho la kwanza kwenye kurasa hii, nina kila sababu ya kuandika au kusema chochote kwa makundi ya watu, nitakuwa mchoyo wa shukrani na fadhila kama nitakaa kimya na kuficha furaha yangu  kwenu,  nafsi yangu itanisuta kama sitakuwa mkweli kuhusu hili, miaka miwili kwangu mimi ni sawa  na zawadi, hatua kubwa, mafanikio na chachu ya kusonga mbele katika kutimiza tamaa zangu…..

Wadau wa ChingaOne blog
Nyie ni kila kitu …….. Toka siku ya kwanza niliyopata wazo la kufanya ninachokifanya nyie mlikuwa chaguo na watu muhimu wa kwanza kuwafikiria, nimetumia muda mwingi kujifunza na kutafuta cha kuwafanya mubaki kuwa wangu, uwepo wenu kwenye kurasa yangu   unaendelea kunipa nguvu na kuona sipotezi muda kwani kuna wengi walio nyuma yangu wanatambua na kuthamini mchango wangu kwao ….. Nawashukuru sana.

Mablogger
Mmekuwa walimu wangu ………… Uwepo wenu katika harakati nzima ya kublogisha umenipa ujasiri, nguvu na ari ya kusonga mbele, wengi ni mashahidi wa mengi yaliyotokea baina yetu  na ninaamini bila hayo ingekuwa ngumu kwangu kufika hapa, Nashukuru kuna baadhi yenu niliweza kuwakonga nyoyo zenu na kukubali ninachofanya na kunipa moyo,  nyie mmenipa nguvu  ya kusonga mbele na kuona naweza kufanya kitu kinachoweza kupendeza kwenye macho na mioyo ya wengine  …. Nawashukuru sana. Kuna wale ambao hawakuweza kuelewa nia na madhumuni yangu  kiasi cha mimi na wao kupishana  macho, ndimi, maono na hata muelekeo ila kiukweli  nyie mmenifundisha kutokata tamaa na kunifanya nirekebishe makosa na kuwa bora zaidi ….. Mungu awabariki.

Familia
Uwepo wenu katika maisha yangu ni chachu ya mafanikio yangu….. Sikujua kama nifanyacho  kinaweza kuwafaurahisha kiasi cha kunipa msaada wowote ninaotaka  kwa muda wowote, mmekuwa mstari wa mbele kunishika mkono tofauti na matarajio yangu, mmekuwa mstari wa mbele kunipa moyo   kwa wakati muhimu ambao nilikata tamaa na kupata magumu. Kwangu  mmekuwa kama LULU  na maji kwa mpanda farasi nyikani, nafasi yenu kwangu ni kubwa kuliko ninavyoweza kuonyesha au kusema ….Asanteni sana na najivunia kuwa nanyi kama wanafamilia.

Marafiki
Najivunia kuwa rafiki yenu…… Miaka miwili hii haikuwa rafiki kwangu na kwenu baada ya mimi kutumia muda mwingi kwenye chingaone kuliko kuwa na nyinyi, najua ilikuwa ngumu kwenu hata kwangu lakini bila kinyongo mlinielewa na kunishika mkono bila kuniacha, uvumilivu wenu na uelewa wenu mlinifanya nigundue nini maana ya urafiki, kwa sababu utoro wangu kwenye baadhi ya mambo yetu umezaa kitu muhimu kati yetu nimegundua urafiki wa kweli, upendo wa dhati na mshikamano, najivunia kuwa wenu.

ChingaOne Team
Mmekuwa nguzo kubwa kwenye jengo langu………. Mimi kama mimi ni ngumu kusonga mbele peke yangu ila msaada wenu umenifanya nifike hapa nilipo. Uwepo wenu katika kuniongezea nguvu ya kufanya chingaone isonge mbele  ni zaidi ya chochote, nawashukuru kwa kunishika mkono na kuwepo na mimi kwa kipindi ambacho nawahitaji sana….. Mungu awazidishie nguvu, utashi na mshikamano.

Post a Comment

 
Top