Menu
 

 Sehemu ya Mifuko ya Mbolea kimeo ikisogezwa pembeni na vijana wa kazi baada ya kufunguliwa kwa dula la Mbolea la STACO LTD na kusafishwa kwamba mbolea nyingine haina matatizo

 Mbolea yenye alama ya kampuni ya YALA aina ya DAP ambayo pia imekutwa ikiwa chini ya kiwango

ofisa wa Upelelezi Mbozi akionyesha sehemu ya Mbolea mbovu ambayo imefumbiwa macho na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania na kuitakatisha kama haina matatizo wala madhara kwa wakulima


Katika hali inayoonyesha kuna mchezo mchafu wa kuendelea kuwamaliza wakulima wilayani Mbozi, shehena ya Mbolea mbovu iliyozuiwa  kuuzwa mwaka jana hatimaye “upepo umepita” na kuruhusu iendelee kuuzwa kwamba ipo juu kiviwango!

Katika hali hiyo wakulima wamekuja juu jana wakati wakishuhudia ufunguzi wa duka la STACCO ambalo miezi kadhaa lilishuhudiwa likiwa limepigwa makufuli na kwa mbwembwe nyingi ikiwemo msururu wa vyombo vya habari, lakini kwa jana ilikuwa kimya kimya kufuli la kwanza likafunguliwa, likafuata la pili na hatimaye la tatu!

Wakati wananchi kwa macho yao meupe wakishuhudia mifuko iliyoganda ya Mbolea za UREA, DAP, CAN na SA taarifa iliyotolewa kuruhusu kufunguliwa kwa duka hilo inatoa maelezo kuwa ni Mbolea ya SA peke yake  ndiyo iliyobainika kuwa na ubora hafifu! ambayo ni mifuko 11 tu.

Hata hivyo afisa anayesimamia ubora wa Mbolea katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi Bi Shonyela amesema licha ya maelekezo kutoka juu mengine hayatatekelezeka kwani kufanya hivyo itakuwa ni kuwamaliza wakuliwa wa wilaya yake kwakuzingatia kuwa Mbolea iliyoganda kuto kufaa tena mashambani.

“nimeandikiwa Mbolea aina ya SA pekee ndiyo isafirishwe chini ya usimamizi wa polisi kwenda Dar es Salaam lakini ni mifuko 11tu! Wakati kuna mbolea aina nyingine ambazo ni zaidi ya mifuko 50 hazina viwango vya ubora na taarifa imekuwa kimya” alifafanua

Uchunguzi wa haraka kwenye duka hilo unaonyesha kuwa mifuko16 ya DAP ilikuwa imeganda wakati wa kufunga duka hilo mwezi September mwaka jana, UREA mifuko 16, CAN 11 na SA 11.

Ingawa katika maelezo ya mkurugenzi wa Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA ilionyesha kuwa wangeshirikiana bega kwa bega na TBS katika kuhakikisha viwango vya bidhaa hiyo vinasimamiwa, maamuzi ya kuruhusu uuzwaji wa mbolea aina ya DAP, CAN na UREA iliyoharibika kwenye ghala la STACO wilayani Mbozi yanajenga mawimbi na mashaka kwa wananchi kuwa mamlaka imelainishwa na ama wamefumbishwa macho!

Tanzania hutegemea maabara yake ya Mbolea iliyopo Mlingano mkoani Tanga kuthibitisha ubora wa bidhaa hizo hata hivyo kumekuwepo udanganyifu unaofanywa na baadhi ya maofisa wa serikali na kuwasaliti wakulima kutokana na makampuni yanayofanya shughuli za usambazaji wa pembejeo na hasa Mbolea kushika keki kubwa katika mzunguko wa fedha nchini

Wakati pia chuo cha kilimo SUA kimekuwa kikitumika katika tafiti na uchunguzi wa Mbolea, mwaka jana Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika Dr Adam Malima alikataa matokeo ya uchunguzi wa mbolea yaliyotolewa na SUA na kuahidi sampuli za Mbolea iliyokamatwa RUVUMA kupelekwa nchini Afrika kusini kujiridhisha na uchuguzi wa maabara za huko baada ya kulalamikiwa na wakulima

Aidha naibu waziri alisitisha leseni za makampuni ya STACO na Mohamed Enterpries mnamo August 07 mwaka jana, ambapo baada ya siku kadhaa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania Suzana Ikelya alitua Mbozi na kukamata Mbolea kwenye duka la STACO

“Maamuzi ya mamlaka ya ukaguzi wa ubora wa Mbolea yanawaacha wananchi wilayani Mbozi wakikosa imani kutokana na namna maamuzi yanavyofikiwa hata katika mambo ambayo hayahitaji utaalamu kuthibitisha ubora kama suala la Mbolea iliyoganda” anaeleza bwana Keneth Mwazembe mmoja wa wakulima wakubwa wilayani Mbozi.

Msimamizi wa duka la STACO bwana Julius Masai licha ya kufurahia kufunguliwa kwa ofisi yake ya chakula, amesema ni kweli kwamba kuna mbolea ambayo haimo kwenye barua ya kuruhusu uuzwaji ambayo haifai kwa matumizi lakini wanatumia busara kuitenga licha ya kutoelezwa kwenye barua hiyo

Ni kweli kuna mifuko kama 37 hivi ya mbolea mchanganyiko ambayo ni mbovu na tumeitenga pembeni na hatutaiuza” alisema meneja huyo bwana Julius Masai

Duka hilo limefunguliwa jana chini ya usimamizi wa maofisa wawili wa idara ya upelelezi ya jeshi la polisi na ofisa anayesimamia ubora wa MBOLEA wilaya ya Mbozi, na shughuli hiyo imefanyika kimya kimya tofauti na mbwembwe zilizofanyika wakati wa kufunga duka hilo ambapo wananchi waliokuwa wakipita barabarani waliitwa kushuhudia namna wanavyotendwa!

Kwahisani ya Indaba Africa

Post a Comment

 
Top