Menu
 

Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Wananchi wa Wilaya ya Chunya Mkoani hapa wameulalamikia Uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kutowajengea Soko kwa ajili ya kufanyia biashara zao kutokana na kubomolewa kwa soko lililokuwepo awali ili kupisha ujenzi wa soko la kisasa.
Wananchi hao waliwaambia Waandishi wa Habari kuwa Soko la Awali lilibomolewa Miaka minne iliyopita lakini tangu kipindi hicho Serikali ya Halmashauri ya Wilaya haijafanya juhudi zozote wala kuwaonesha sehemu nyingine ya kufanyia biashara licha ya kusimika nguzo zinazoashiria ujenzi kuendelea kwa muda mrefu.
Walisema hali ya biashara ni ngumu kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuuzui bidhaa zao majumbani na wengine kuchanganya bidhaa za vyakula na vifaa vya ujenzi na vipodozi katika duka moja hali inayohatarisha afya za wakazi hao.
Mwenyekiti wa Soko la zamani, Emmanuel Mwaijumba alisema kutokana na kukosekana kwa soko hakumumizi Mwananchi peke yake lakini pia Halmashauri inakosa Fedha kutokana na kutokuwepo kwa ushuru wa soko kutoka kwa wafanyabiashara.
Alisema kufuatia kukosekana kwa soko hilo walipeleka malalamiko yao kwa Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya hiyo lakini hakuna majibu yoyote licha ya wenye vibanda vinavyozunguka lililokuwa soko la zamani kuendelea kutozwa fedha.
Aliongeza kuwa mbali na kubomolewa kwa soko hilo vibanda vilivyopo havina eneo la vyoo hali inayosababisha usumbufu kwa wenye nyumba jirani na maeneo hayo kutokana na watu wengi kuomba huduma ya choo, pia uwepo wa ghuba la taka eneo hilo kutozolewa kwa muda mrefu ambapo zimekuwa zikichomewa hapo hapo na kuleta adha kwa wamiliki wa Hoteli za jirani kutokana na uchafu, harufu mbaya na moshi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Deodatus Kinawiro alipo pigiwa Simu kuzungumzia suala hilo alikiri kuwepo kwa tatizo na kuongeza kuwa suala hilo lipo kwenye mchakato wa kushughulikiwa hivyo wananchi wawe na subira.

Post a Comment

 
Top