Menu
 

Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Warembo walioshiriki shindano la kumtafuta Mwanamitindo bora wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wamewalalamikia waandaaji wa Shindano hilo kwa kuwapa zawadi finyu tofauti na walivyokuwa wameahidiwa kabla ya kuanza mashindao.
 
Mashindano hayo yalifanyika Machi 30, Mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano wa Mkapa uliopo Sokomatola Jijini Mbeya yaliyoandaliwa na kampuni ya Tanzania Youth Arise kutoka Dar Es Salaam na kuhusisha  wasichana  25.
 
Malalamiko ya warembo hao yanatokana na zawadi walizopewa washindi kuwa kiduchu tofauti na walivyoahidiwa kabla ya kuanza mashindano ambapo inadaiwa kuwa mshindi kwanza alitakiwa kupewa zawadi au kitu chenye thamani ya Shilingi Milioni Moja na Laki mbili (1,200,000/=) lakini mwisho wa mashindano mshindi wa kwanza alipewa Kompyuta ndogo (Mini Laptop) inayokadiliwa kuwa na thamani ya Shilingi Laki nne na nusu( 450,000/=).
 
Wakizungumza na gazeti hili baada ya kukamilika kwa mashindano hayo Warembo hao walisema   Zawadi hizo haziridhishi kutokana na maandalizi waliyoyafanya ambapo mbali na mshindi wa kwanza kupewa kitu hicho pia msindi wa pili alipewa Seti moja ya meza ya chakula yenye thmani ya Shilingi Laki nne (400,000/=).
 
Msindi wa tatu hadi mshindi wa tano wote kwa pamoja na washindi wa kwanza na  pili walipewa zawadi za Mkusanyiko wa mapambo ya kike kutoka kampuni ya Oriflame ambayo thamani yake haikujulikana  huku washiriki wengine 20 walionekana kusuasua katika Hotel ya Manyanya waliokuwa wameweka kambi kutokana na kutopewa kifuta jasho chochote.
 
Jullieth Sillo (20) ambaye aliibuka mshindi wa kwanza alisema licha ya zawadi kutokuwa za uhakika lakini ubabaishaji unaonekana uko kwa waandaaji ambao walishindwa kujipanga mapema ambapo waliahidi kutoa zawadi ambazo hawakuwa na uhakika nazo.
 
Aliongeza kuwa wakati mwingine wadhamini wanatakiwa watoe fedha na vitu mapema kabla ya kuanza kwa mashindano na matangazo ambapo alisema wanatangazwa sana tofauti na vitu wanavyotoa mwishoni au siku ya mashindano.
 
Mbali na hilo Mshindi huyo alisema ukumbini alikabidhiwa Fedha taslimu shilingi Laki tano kiasi ambacho alipokonywa na mratibu wa mashindano hayo kwa kilichidaiwa kuwa haikuwa sehemu ya zawadi bali alikuwa anakamilisha sehemu ya mkataba wa udhamini ambayo ilitolewa na kampuni ya Pepsi.
 
“ Kuhusu kambi ilikuwa ni nzuri maana tumejifunza mambo mengi ambayo ni ushirikiano na watu kufanya huduma za kijamii pamoja na kujitambua” alisema Lilian WilBroad ambaye alikuwa mshindi wa pili.
 
Kwa upande wake Mratibu wa mashindano hayo Bahati Mwakalinga, alipotafutwa ili kujibu tuhuma hizo za kuwapokonya zawadi washindi pamoja na kutoa kiwango kisichoridhisha kwa washiriki na washindi alisema tatizo hilo ni kweli limejitokeza lakini halikusababishwa nay eye bali ni wadhamini walioshindwa kutoa kile walichokuwa wamekiahidi.
 
Alisema sababu nyingine inatokana na watu kushindwa kuingia kwa wingi ukumbini hali iliyosababisha kupata kipato kidogo Mlangoni hivyo kushindwa kumudu gharama mbali mbali kama kutoa kifuta jasho kwa washiriki wote ambao walitakiwa kupewa kila mmoja Shilingi 25,000/= lakini kutokana na kukosa fedha Mratibu huyo aliwaahidi washiriki kutumia fedha hizo baada ya Wiki mbili.
 
Alisema suala la wadhamini ni gumu na ndiyo waliochangia kuvuruga utaratibu ambapo wamekuwa wakitoa ahadi kubwa lakinimwisho wa siku wanashindwa kutekeleza kile wa;lichokiahidi mwanzoni kabla ya Mashindano.
 
Mwakalinga aliongeza kuwa baadhi ya zawadi siyo rafiki kwa washiriki ambao wengi wao ni wanafunzi ambapo Msindi wa Pili ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu (TIA) tawi la Mbeya ambaye alikabidhiwa seti moja ya meza ya Chakula ambayo haitamsaidia kama Mwanafunzi.
 
Aliwataja washindi kuwa ni Mshindi wa Kwanza ni Julieth Sillo kutoka Mbeya, wa pili ni Dinah James Kutoka Mbeya, wa tatu ni Herieth Ferera kutoka Mbeya , nne Lilian Wilbroad kutoka Mbeya na nafasi ya tano ilichukuliwa na Karesma Fredy kutoka Katavi.
 
Aliwataja wadhamini kuwa ni Kampuni ya Vinywaji ya Pepsi, Access Computer Limited waliotoa zawadi kwa mshindi wa kwanza, Global Star waliotoa zawadi kwa mshindi wa Pili ya meza ya chakula( Coffee table) na Oriflame waliotoa bidhaa za mapambo ya wanawake kwa ajili ya washindi wote watano.

Post a Comment

 
Top