Menu
 

Timu ya Taifa ya soka ‘Taifa Stars’ ipo kwenye mashindano ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil mwaka 2014.

Katika Afrika, Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kundi C kati ya makundi 10. Kundi C linajumuisha timu za Ivory Coast, Morocco, na Gambia.

Kwa sasa katika Kundi C, Taifa Stars inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, Morocco ina pointi mbili na Gambia ina pointi moja.

Kwa hali ilivyo hivi sasa, Taifa Stars ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2014, lakini ili Tanzania ifuzu fainali hizo inatakiwa ishinde mechi zote tatu zilizobaki na kuongoza kundi C na baadaye iingie katika timu kumi bora ili baadaye zishindane na zipatikane timu tano kutoka Afrika ambazo zitafuzu kwenda Brazil katika Fainali za Kombe la Dunia 2014.

Kutokana na Taifa Stars kufanya vizuri katika hatua ya makundi na kubakisha mechi tatu dhidi ya Morocco, Ivory Coast na Gambia, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara ameunda Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde.

Wajumbe wa Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Singida Mjini, Mohammed Dewji, ni Teddy Mapunda, Dk Ramadhani Dau, Dioniz Malinzi, Asji Shabir, George Kavishe, Mohammed Raza (Mbunge), Leodger Tenga, Joseph Kusaga, Kapteni John Komba na Zitto Kabwe (Mbunge).

Kamati hiyo baada ya kuteuliwa ilitakiwa na waziri kuanza kazi mara moja na iliambiwa hadidu za rejea zitakazowaongoza kutekeleza majukumu yao watazipata Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Pia, Serikali iliahidi kutoa ushirikiano utakaohitajika kwa kamati hiyo ambayo inaundwa na wadau mbalimbali wa soka ili ifanye kazi iliyopewa vizuri na kuiwezesha Taifa Stars kushinda mechi zote zilizobaki. Sisi tunaitakia kila la kheri Kamati hiyo ya kuisadia Taifa Stars ishinde kwani tunaamini imeundwa kwa dhamira ya dhati na katika muda mwafaka wa kuisaidia Taifa Stars.

Tunasema hivyo kwa sababu hivi sasa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaelekea ukingoni mwezi huu, ambapo kamati hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na benchi la ufundi la Taifa Stars wanatakiwa kuhakikisha wachezaji watakaoteuliwa kuunda kikosi cha Taifa Stars wanaingia kambini mapema kwa ajili ya maandalizi ya mechi zake za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwezi Juni.

Taifa Stars haijawahi kucheza Fainali za Kombe la Dunia zaidi ya kuishia hatua za awali za kufuzu, lakini kama mikakati ikiandaliwa kikamilifu, nafasi hiyo ipo.

Sisi tunaamini kuwa Taifa Stars ikipata ushindi katika mechi dhidi ya Morocco na Ivory Coast, ushindi huo utafufua na kutia chachu nafasi ya Tanzania kufika mbali katika mashindano hayo ya kufuzu.

Kinachotakiwa kufanywa hivi sasa ni kamati hiyo ya kuisaidia Taifa Stars ishinde kutafuta fedha za kutosha, ambapo zikiunganishwa na fedha za wadhamini wa Taifa Stars basi Taifa Stars itapata maandalizi mazuri ikiwamo kuweka kambi nje ya nchi.

Pia tunaamini kocha wa Taifa Stars atachagua wachezaji wenye uwezo, uzalendo wa hali ya juu, umoja na kujenga lengo moja la kutafuta ushindi.

Tunaamini Kamati ya kuisadia Taifa Stars kushinda itafanya kazi zake kwa bidii na kufuta dhana ambayo imejengeka katika jamii kuwa kamati hiyo haina umuhimu.Text inakuja hapa.

Post a Comment

 
Top