Menu
 

Ndugu zanguni
Kwanza kabisa napenda kuelezea masikitiko yangu juu ya tukio lililomkuta Mwandishi mwenzangu veteran wa tasnia hii Kassim Mikongoro. Nampa pole sana kwa sababu yaliyomkuta katika ghasia za Mtwara sio tu yamempa hasara ya Mali bali pia yamemuathiri kisaikolojia yeye na familia yake. Niwe mkweli hata mimi nimeathirika kisaikolojia kutokana na tukio lilimkuta Kassim. Na kwa mara nyingine Pole sana Kassim.

Haya yamemkuta Kassim lakini mimi naamini yanaweza kumkuta mwandishi wa habari mwingine yeyote, nasema hivi kwa sababu nina shauku ya kuamsha mjadala utakaosaidia kuangalia mustakabali wa waandishi wa habari katika usalama wao na familia zao. Najua kwa yaliyomkuta Kassim kila mtu anaweza kusema la kwake lakini ni vizuri kukumbushana kuwa tukiweka kando hisia hizo zote Kassim ni mwandishi wa habari kama alivyo mwandishi wa habari mwingine yeyote.

Nionavyo mimi swali hili tunapaswa kujiuliza sote wadau, nikiwa na maana waandishi wa habari wenyewe, wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri wa habari, mamlaka za kiserikali na wananchi ambao tunawahudumia. Kwa namna yoyote ile si haki kuwashambulia waandishi wa habari, tena wasihukumiwe kienyeji namna hiyo. Tukifikia hapo na kwa kuwa Mhimili wetu sio rasmi basi naona huku mbeleni itakua kila asiyeridhishwa na kazi zetu anatuadhibu kwa namna alivyoadhibiwa Kassim. Atabaki nani?

Ni vizuri tulijadili hili kwa weledi na busara na wananchi wajue tuna maana gani. Mimi ni miongoni mwa waandishi wa habari walikutana na mikutuo ya kutishiwa, wakati mwingine kushambuliwa na hata kupigwa kutokana na kazi ya uandishi wa habari. Nakumbuka wakati nasoma chuo kikuu Mwalimu wangu aliwahi kuniambia kuwa siku zote Ukiandika habari hasa yenye sifa na mvuto wa kuwa habari wapo utakaowafurahisha na wapo utakaowakwaza. Nilivutiwa sana na somo hili na nikajiridhisha pasipo mashaka kuwa kumbe kwa waandishi wa habari kukwaza watu kila siku ni sehemu ya maisha yetu katika kazi hii. Matharani ukiandika habari juu ya mpango mzuri wa kuwawezesha wakulima kuzalisha chakula cha kutosha kwa namna yoyote utakua umewafurahisha wakulima lakini pia utakua umewakwaza wafanyabiashara ambao biashara zao zinategemea wakulima wakose chakula cha kutosha ili wao waingize chakula kutoka nje ya nchi na wapate mapesa lkuki ya faida. Hali kadharika ukiandika habari inayohimiza nchi kuishi kwa amani utakua umewafurahisha wanaopenda amani na utakua umewakwaza wanaotamani amani ipotee ili mipango yao ifanikiwe. Ipo mifano mingi. Yaliponikuta ya kushambuliwa wakati nikifanya kazi ya kuripoti hali ya vituo vya kura kuwa shwari baada ya zoezi la upigaji kura ilihali kuna watu walitaka kusiwe na amani kengele iligonga kuwa hizi ndio changamoto za uandishi wa habari.

Sasa mimi najiuliza swali hivi kama kila mtu ambaye hafurahishwi na habari zetu atachukua jukumu la kutushambulia kama ilivyokua kwa Kassim Mikongoro, atabaki nani?

Saa chache baada ya nyumba ya Kassim Mikongoro kuchomwa moto, nimeongea nae kwa njia ya simu, nilishindwa kujizuia na machozi yamenitoka pale kaka yangu huyu ambaye ametumikia kazi hii kwa karibu miaka 40 tena kwa habari, vipindi, makala na ripoti nyingine mbalimbali za kuelimisha wananchi juu ya maendeleo yao ya Kilimo, ustawi wa jamii nakadharika aliponiambia kuwa yaliyomkuta yamesababisha aanze kufikiria kuanza maisha upya kwa sababu kila kitu kimeteketea kwa moto na nilipokua nikizungumza nae ameniambia amebakiwa na pensi na shati moja tu alivyovaa. Imeniuma saaaana saaaana.

Ikaniuma zaidi aliponithibishia kuwa kwa kuwa alijua kuwa ajenda ya gesi imekaa vibaya, katika ripoti zake aliepuka kujihusisha na habari zinazohusiana na gesi. Kwa kuwa alijua hatakua salama endapo atajihusisha na jambo hili. Sijajua waliomhukumu walitumia vigezo gani na wamemhukumu kwa kosa gani Kassim, mtu ambaye amekua mstari wa mbele kuwapigania wakulima wa korosho wa Mtwara, kupigania hali mbaya ya miundombinu ya Mtwara, aliyetengeneza makala kadhaa za kutangaza fursa za Mtwara, ambaye amekua tayari kufanya kazi Mtwara mahali ambako waandishi wa habari wengi hukataa kupangwa huku kufanya kazi kutokana na changamoto za maisha za Mtwara. Siwezi kusema yote hapa. Ila itoshe kusema POLE SANA KASSIM MIKONGORO.

Anyway wadau tuliangalie hili.

Na kwa wakati huu naomba tusisite kumchangia mwenzetu Kassim Mikongolo ili maisha yake yaendelee, tumchangie fedha Jamani na napendekeza tuwe na utamaduni huu ili tutiane moyo kwa kuwa usalama wa waandishi wa habari katika nchi yetu umejaa maswali mengi. Na tukumbuke nchi yetu inatajwa kushika nafasi ya tatu barani Africa kwa waandishi wa habari kuwa hatarini

Pole sana Kassim, nipo na wewe katika wakati huu Mgumu and Please be strong brother.
 
Imeandikwa na  Gerson Msingwa

Post a Comment

 
Top