Menu
 

TAARIFA iliyotua kwenye dawati la gazeti hili hivi karibuni inaeleza kuwa, mavazi yasiyo ya heshima vikiwemo vimini yamepigwa marufuku...
 
Kuvaliwa na wasanii kwenye filamu wanazorekodi na yoyote atayekiuka atakiona cha mtemakuni.Chanzo chetu makini kilichoomba hifadhi ya jina lake, kimeeleza kuwa waliotoa agizo hilo ni Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Filamu lengo likiwa ni kuhakikisha maadili ya taifa yanazingatiwa.
 
Ikaelezwa kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia uwepo wa filamu nyingi mtaani ambazo wasanii wanaoshiriki huvaa mavazi yasiyo ya heshima, mazingira yanayoiharibu jamii. 

“Kama wanavyosema vijana huko mtaani kwamba kimenuka na kweli kimenuka! Sasa hivi vimini ‘no’ kwenye filamu, bodi ya filamu imeona ilivalie njuga suala hili ili kulinda maadili ya taifa,” kilieleza chanzo hicho.


Katika kujua ukweli wa jambo hili, mwandishi wetu alimtafuta Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba ambaye alikiri kuwepo kwa utaratibu mpya wa Bodi ya Filamu wa kuzipitia filamu zinazoingia mtaani na kwamba zinazokiuka maadili zinafungiwa. 
 
Mwakifwamba alisema ni kweli mavazi ya nusu utupu hayataruhusiwa tena kuonekana kwenye filamu kama ilivyokuwa huko nyuma na wale watakaojifanya vichwa ngumu watashughulikiwa.

“Sasa hivi kuna sheria mpya kabisa, hakuna kuvaa nguo zisizo za maadili na ukikiuka basi filamu yako haioneshwi au kama unaweza urudie na kuondoa vipande vilivyoharibu filamu hiyo,” alisema Mwakifwamba huku kukiwa na maelezo kuwa, hilo pia litasimamiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya Waziri Fenella Mukangara.

Post a Comment

 
Top