Menu
 

Wanawake wa Kata ya Mshewe Wilaya ya Mbeya vijijini wakijadiliana namna ya kuanzia na kuendesha vituo vya taarifa na maarifa katika warsha iliyo endeshwa kwa siku mbili na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kumalizika jana.

Na Pendo Omary, Mbeya Vijijini
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeendesha warsha ya siku mbili kuhusu namna ya kuanzisha na kutumia vituo vya taarifa na maarifa katika kata ya Mshewe, wilaya Mbeya Vijijini yaliyomalizika jana. Mafunzo hayo  kwa vikundi vya wanawake yalikuwa ni mwendelezo wa mafunzo ya  uraghbishi yaliyofanyika hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya kuendeleza harakati za ujenzi wa vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi lililojikita katika ngazi za jamii.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo toka TGNP Kenny Ngomuo alisema, malengo ya mafunzo hayo ni pamoja na kushirikishana  katika kujenga uelewa wa dhana ya kituo cha taarifa na maarifa, kuoanisha yaliyojiri katika zoezi la uraghibishi na uanzishwaji wa kituo cha taarifa na maarifa.

“Malengo mengine ni kujifunza namna ya kuanzisha na kuendeleza vituo vya taarifa na maarifa na kuoanisha fursa zilizopo na kutengeneza mpango kazi wa kituo pamoja na ufuatiliaji,” alisema Kenny.

Alisema Vituo vya maarifa na taarifa vitaleta chachu ya kuzidi kukita harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi ya jamii. Vituo hivi vitachochea ujenzi wa nguvu za pamoja  Katika jamii ya kata ya Mshewe kwa kutumia mikakati kama  kukusanya, kutumia na kusambaza maarifa na taarifa.

Pia kuendesha mijadala ya wazi na kuweka kumbukumbu kuhusu mijadala hiyo, kuendesha mafunzo mbali mbali na kuweka kumbukumbu kuhusu mafunzo hayo, kufanya uchambuzi na ufuatiliaji wa masula au kero zinazoikabili jamii ya Mshewe; na kuchukua hatua za pamoja  kukabiliana na kero hizo.

 “Kutokana na uzoefu uliojitokeza katika vituo tulivyovianzisha mwaka jana katika kata Sogwa, wilaya ya Kishapu, kata ya Mkambarani, wilaya ya Morogoro Vijijini na kata ya Ijombe wilaya Mbeya Vijijini, imeonyesha kuwa vituo tulivyovianzisha wanawake wamevitumia katika kuibua mambo mbalimbali yakiwemo masuala ya, afya, maji na umiliki ardhi na vimekuwa mkombozi wa wanawake katika kufuatilia masuala yanayowagusa,” aliongeza Kenny.

Aidha washiriki wa warsha hiyo walisema, wamejifunza namna ambavyo watatumia vituo hivyo katika kupashana habari na kubadilishana uzoefu wa shughuri wanazozifanya ikiwemo uzalishaji mali ili kuongeza ozoefu.

“Kupitia kituo cha taarifa na maarifa, nitaweza kujua namna ya kudai haki zangu na za wengine hasa walioko pembezoni na kuhamasisha jamii na uongozi kuitisha mikutano na kujadili namna ya kutatua changamoto zinazotukabili hasa sisi wanawake,” alisemaMelise Nkembo kutoka kijiji cha Mshewe, kata ya Mshewe.

Aidha Witness Sikayanga kutoka kijiji cha Mshewe, kata ya Mshewe alisema kupitia mafunzo hayo watahamasisha jamii na kuwapa elimu itakayowasaidia kuunda vikundi mbalimbali na kuanzisha vituo hivyo ili kusambaza vuguvugu la ukombozi wa wanawake na makundi yaliyoko pembezoni.
“Tunapaswa kwenda kwenye jamii na kuwapa haya mafunzo ili kuendeleza harakati za ukombozi wa wanawake na wote waliopembezoni. Tunaiomba TGNP Kuendelea kutoa mafunzo haya kwa watu wengine,” alisema Witness.
Short URL: http://www.thehabari.com/?p=33318

Post a Comment

 
Top