Menu
 

Baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Sudan, kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars kimeondoka mjini Adis Ababa nchini Ethiopia, kuelekea mjini Marrakesh nchini  Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.

Taarifa iliyotolewa na Afisa habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF Boniface Wambura, imeeleza kwamba kikosi cha Stars kimeondoka mjini Adis Ababa mishale ya alfajiri na kilitarajiwa kuwasili mjini Casablanca nchini Morroco mishale ya saa 8 mchana.

Kabla ya kuondoka mjini Adis Ababa, kikosi cha Stars jana jioni kilialikwa chakula cha usiku na balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro, ambapo kilikutana pia na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia.

Katika hafla hiyo ya chakula cha jioni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro aliwataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanacheza kwa kujituma katika mchezo dhidi ya timu ya taifa ya Morocco kwa ajili ya kuendeleza wimbi la ushindi.

Ombi hilo la Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro kwa wachezaji wa Taifa Stars linakwenda sambamba na lile lililotolewa na raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete wakati alipowaalika chakula cha mchana wachezaji wa timu hiyo  May 24.

Stars wameelekea Morocco wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao matatu kwa moja walioupata katika mchezo wa kuwani kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 uliochezwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam March 24 mwaka huu.

Wachezaji walioelekea nchini Morocco ni nahodha Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi huku washambuliaji Mbwana Sammata pamoja na Thomas ulimwengu wakitarajia kuunga na wenzao ndani ya juma hili.

Post a Comment

 
Top