Menu
 

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Bibi Fatma Mwassa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami katika mkoa huo umekuwa ukisuasua kwa sababu wakandarasi wanaofanya kazi hizo hawajalipwa fedha zao na wanaidai Serikali karibu sh. bilioni 44/-.

Ametoa kauli hiyo jana mchana (Alhamisi, Agosti 29, 2013) wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika mkoa wa Tabora mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye aliwasili mkoani humo kwa ziara fupi ya siku mbili.

Alisema mkoa huo una wakandarasi watano ambao wanatekeleza kazi za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami lakini ujenzi huo uko nyuma kinyume na mkataba kwani viwango vya ukamilikaji vinatofautiana kuanzia asilimia 19 hadi asilimia 41.

“Kwa mujibu wa muda uliowekwa katika mikataba ya makubaliano ya ujenzi wa barabara, miradi karibu yote iko nyuma ya wakati wa kukamilika kwa miradi hiyo. Ni matumaini ya mkoa kuwa Serikali itaendelea kutoa msukumo ili kuhakikisha kuwa miradi yote hii inakamilishwa katika muda mfupi ujao, na kikubwa ni kulipwa kwa deni la sh. bilioni 44/- ambalo Serikali inadaiwa na wakandarasi hawa,” alisema.

Alizitaja barabara ambazo ujenzi wake unasuasua kuwa ni Tabora-Nzega, sehemu ya Nzega – Puge (km.58.8) na sehemu ya Puge – Tabora (km. 56.1); Tabora-Nyahua-Chaya (km.85); Tabora – Urambo sehemu ya Tabora-Ndono (km.42) na Ndono –Urambo (km.51) ambazo zote pamoja gharama yake ni sh. 333,608,309,496/-.

Mkoa w tabora una mtandao wa barabara wenye jumla ya km2,943.3 zinahudumiwa na wakala wa barabara (TANROADS) ambapo km. 965.8 ni barabara kuu na km. 1,977.54 ni barabara za mkoa. Kati ya hizo, km. 158 ni lami na km. 2,784 ni za changarawe na udongo.

Akizungumzia kuhusu mapato ya mkoa huo, Bibi Mwassa alimwomba Waziri Mkuu asikubali kusikiliza maneno ya watu wanaotaka ushuru wa mazao (Procude CESS) uondolewe kwani wanaodai hivyo hawaitakii mema Tanzania.

“Tunaomba Produce CESS isifutwe, tunajua faida yake, tunaomba ibaki ili iweze kuzisaidia Halmashauri za hapa nchini. Hapa Tabora kwa kutumia fedha ya CESS ambayo ni asilimia tano, tumefanya mambo mengi. Mfano Kaliua wametenga sh. bilioni 1.2/- za kujenga ofisi za wilaya, Sikonge wameweza kutenga fedha za mradi wa kijiji cha vijana, wamejenga theatre, sehemu ya kufulia na wodi ili kukiwezesha kituo cha afya kiwe hospitali ya wilaya,” alisema.

“Tunaomba Produce CESS isifutwe, tunajua faida yake, tunataka ibaki ili iweze kuzisaidia Halmashauri za hapa nchini. Hapa Tabora kwa kutumia fedha ya CESS ambayo ni asilimia tano, Kaliua wametenga sh. bilioni 1.2 za kujenga ofisi za wilaya, Sikonge wameweza kutenga fedha za mradi wa kijiji cha vijana, wamejenga theatre, sehemu ya kufulia na wodi ili kukiwezesha kituo cha afya kiwe hospitali ya wilaya,” alisema.

Akitoa nasaha zake kwa viongozi mbalimbali wa mkoa waliofika kumpokea na kusikiliza taarifa hiyo, Waziri Mkuu Pinda aliwaomba waitunze tunu ya amani na utulivu iliyomo mkoani humo kwa sababu mawazo mazuri ya kuendeleza mkoa wao hayawezi kufanikiwa kama wataruhusu vurugu zitokee.

Aliwaelekeza Mkuu wa Mkoa na timu yake waweke utaratibu mzuri wa ushirikishwaji hasa kwa viongozi wa dini mbalimbali kwani nao pia ni walezi wa wananchi wale wale ambao viongozi wa mkoa na wa kisiasa wanawaongoza. “Kazi kubwa kwetu sote ni kuitoa Tanzania hapa tulipo na kuipeleka mbele zaidi,” akiongeza.

“Najua kuna RCC lakini haitoshi kwa sababu wanaohudhuria ni wachache na wana nyadhifa maalum. Tafuta siku muandae mjadala kuhusu uwekezaji. Waite viongozi wa dini wa wilaya na wa mkoa, waiteni wananchi kadhaa kuwe na ushiriki mkubwa na wa tofauti. Mtapata maoni yao lakini pia mtakuwa mmefikisha taarifa kwa wananchi kuhusu nini kinafanyika katika mkoa wao,” alisema.

Post a Comment

 
Top