Menu
 

 

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                                    01 Februari, 2014


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Jaipur,India

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewasili nchini India kuanza ziara ya kikazi ya siku tisa nchini humo.

 

Dk. Shein aliwasili New Delhi mapema asubuhi ambapo aliunganisha ndege hadi katika mji wa Jaipur Makao Makuu ya Jimbo la Rajastan ambako jioni anatarajiwa kuanza ziara yake kwa kutembelea eneo la kihistoria la makumbusho ya ngome ya Amber.

 

Ziara hiyo ina lengo la kukuza uhusiano kati ya Tanzania na India pamoja na kuhimiza ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya India katika maeneo ya kiuchumi, huduma za jamii, biashara na uwekezaji.

 

Katika ziara hiyo Dk. Shein atafanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo pamoja na jumuiya za wafanyabiashara kwa madhumuni ya kuimarisha ushirikiano uliopo pamoja na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo uwekezaji na uimarishaji wa biashara ya utalii kati ya India na Zanzibar.

 

Kwa mujibu wa ratiba kesho Jumapili tarehe 2 Februari, 2014 atatembelea Chuo cha Barefoot kilichoko katika kijiji cha Tilonia, wilaya Ajmer katika jimbo hilo.

 

Akiwa chuoni hapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatia saini makubaliano ya ushirikiano na chuo hicho ambacho kinatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiuchumi, kijamii na kielimu wanawake wazee na wajane waishio vijijini ili kuinua kiwango chao cha maisha.

 

Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na Mke wake Mama Mwanamwema, Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Zainab Omar Mohamed, Waziri wa Biashara na Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Marzui, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim na Balozi wa Tanzania nchini India Injinia John Kijazi.

 

Wengine katika msafara huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Mohamed Saleh Jidawi na Katibu Mkuu Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim, Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar –ZIPA Salum Khamis Nassor.

 

Keshokutwa Jumatatu mapema asubuhi atazuru kumbukumbu ya Mahatma Ghandhi ambako ataweka shada la maua na baadae atafanya mazungumzo na Mwenyeji wake Makamu wa Rais.

 

Baadae mchana siku hiyo atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa India Bwana Manmohan Singh, ataonana na Waziri anayeshughulikia Diaspora na Waziri wa Afya na Familia wa nchi hiyo. Jioni atakutana na watanzania wanaioshi Delhi na baadae usiku atahudhuria chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa heshma yake na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa India.

 

Tarehe 4 Februari, 2014 atatembelea kituo cha utafiti wa mazao ya kilimo, atakutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara na kuondoa kwenda mji wa Hyderabad ambako siku inayofuata atakutana na Mwenyekiti wa hospiltali za Appolo na kusaidia Makubaliano ya Ushirikiano.

 

Dk. Shein siku hiyo atakutana pia na Baraza la Biashara ya Madawa Nchi za Nje la India na baadae atapata fursa ya kutembelea kiwanda cha madawa ambapo baadae atasafiri hadi mji wa Bengaluru ambako siku ya Alhamisi tarehe 6 Februari, 2014 atatembelea hospitali ya Manipal na kutia saini makubalino ya ushirikiano na hospitali hiyo na baadae kuondoka kwenda Mumbai.

 

Akiwa Mumbai tarehe 7 Februari, 2014 Dk. Shein atatembelea Kampuni ya kutengeneza matrekta ya Mahindra na baadae jioni atakutana na makampuni ya biashara ya utalii na wakala wa safari za kitalii.

 

Jumamosi tarehe 8 Februari, 2014 Rais na ujumbe wake utatembelea kiwanda cha kusindika viungo (spices) cha Everest ambako pia atakutana na wafanyabishara wa viungo.

 

Rais wa Zanzibar naMwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na ujumbe wake utaondoka India Jumapili tarehe 9 Februari, 2014 kurejea nyumbani.

Post a Comment

 
Top