Menu
 

Na Venance Matinya, Mbeya.
ASKARI wa Jeshi la Polisi na raia mmoja wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Mbeya wakituhumiwa kwa makosa mawili ambayo ni kula njama za kutenda kosa pamoja na wizi wa mtoto.
 
Watuhumiwa hao ni pamoja na Mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa Ditektivu Constebo wa Polisi mwenye namba WP 5367  Prisca Isaya (35) mwenyeji wa Ilala Dar es salaam ambaye hata hivyo alivuliwa vyeo na kufukuzwa kazi kabla ya kupandishwa Mahakamani  na Salehe Mwangosi (28) mkazi wa Njisi wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya.
 
Akisoma mashtaka yanayowakabili Mwendesha mashtaka wa Serikali, Juliana William, mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Mbeya, Maria Batulaine, alisema watuhumiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na makosa mawili waliyoyatenda Aprili 4, Mwaka huu.
 
Alisema kosa la kwanza ni kula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuiba mtoto kinyume cha kifungu cha 384 (16) cha kanuni ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002 walilofanya Aprili 4, Mwaka huu katika eneo la Songwe wilayani Kyela.
 
Alitaja kosa la pili kuwa ni Wizi wa mtoto  kinyume cha kifungu cha 169 (1) (a) sura ya 16 ya kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
 
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia Mahakama kuwa washtakiwa wote kwa pamoja mnamo Aprili 6, Mwaka huu katika eneo la Zahanati ya Njisi Wilaya ya Kyela Mkoani hapa kwa maksudi waliiba mtoto mwenye umri wa siku saba kutoka kwa  mama yake mzazi Mboka Mwakikagile.
 
Washtakiwa wote kwa pamoja walikana kuhusika na tukio hilo ambapo upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na upo tayari kuwaleta mashahidi wake kwa ajili ya kuendelea na usilizwaji wa kesi.
 
Kwa upande wake Hakimu aliahirisha kesi hadi Mei 6, Mwaka huu na kwamba dhamana kwa washtakiwa iko wazi kama watakidhi vigezo ambavyo ni kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizo hamishika zenye thamani ya shilingi Milioni 5, barua ya mtendaji na barua kutoka kwa mwajiri kwa ajili ya mshtakiwa wa kwanza.
 
Hata hivyo walishindwa kuwa na wadhamini waliokidhi vigezo vya mahakama na kuamliwa kurudishwa rumande hadi Mei 6, Mwaka huu kesi itakapo kuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Post a Comment

 
Top