Menu
 


Klabu ya Chelsea huenda ikafaidika na kiasi cha paund million 6, endapo itapangwa na klabu ya Atletico Madrid katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Chelsea wanajipanga kupokea kitita hicho cha pesa, kama wataangukia mkononi mwa Atletico Madrid katika hatua hiyo kufuatia kifungu kilichopo kwenye makubaliano ya klabu hizo mbili wakati The blues wakikubali kumpeleka kwa mkopo mlinda mlango kutoka nchini Ubelgiji Thibaut Courtois huko Estadio Vicente Calderón.

Imeripotiwa kwamba katika makubaliano hayo, kuna kifungu ambacho kipo kwenye mkataba wa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 21 ambacho kinaishurutisha klabu ya Atletico Madrid kutomtumia Thibaut Courtois endapo itatokea wanakutana na Chelsea kwenye michuano ya kimataifa.

Kifungu hicho kimeendelea kusisitiza kwamba endapo Atletico itawalazimu kumtumia kipa huyo itawagharimu kuwalipa Chelsea kiasi cha paund million tatu kwa kila mchezo watakaomtumia Thibaut Courtois.

Kama klabu hizo zitapangwa kukutana katika mchezo wa hatua ya nusu fainali, na Atletico Madrid wakafanya maamuzi ya kumchezesha mlinda mlango huyo katika mchezo wa nyumbani na ugenini, itawalazimu kuwalipa Chelsea paund million 6.

Hata hivyo kitendawili cha Atletico Madrid kupangwa na Chelsea katika mchezo wa hatua ya nusu fainali, kitateguliwa kesho mara baada ya upangaji wa michezo ya hatua ya nusu fainali, ambapo hafla yake itafanyika mijini Nyon nchini Uswiz.

Atletico Madrid wamefanikiwa kutinga katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, baada ya kuifunga FC Barcelona bao moja kwa sifuri katika mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo huko jijini Madrid.

Baada ya ushindi huo klabu hiyo Estadio Vicente Calderón, imesonga mbele kwa jumla ya mabao mawili kwa moja na kuungana na FC Bayern Munich, Chelsea pamoja na Real Madrid ambazo zimetinga kwenye hatua ya nusu fainali.

Post a Comment

 
Top