Menu
 Rapper Mabeste, Januari hii anatarajia kuachia ngoma mpya iitwayo 'Usiwe Bubu' yenye funzo kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao na kujenga urafiki ambao utawafanya watoto kuwa huru kuuliza mambo mbalimbali yanayohusu maisha na kupata haki ya malezi bora kutoka kwa wazazi wao.

''Unakuta mzazi anaogopa kumwambia kitu mwanae kwa sababu anaona ni mapema kumwambia mwanae namna ya kuepukana na mahusiano ya mapenzi ya utotoni na madhara yake pamoja na madhara ya ngono, vilevile namna ya kuepukana na makundi yasiyofaa mfano ujambazi, matumizi ya madawa ya kulevya n.k na baadae kuharibikiwa, lakini kumbe ni vizuri mtoto kuwa na urafiki na mzazi kwa sababu kuna umri wa mtoto kuingia katika mahusiano wa kimapenzi lazima awe na urafiki na mzazi wake ili mzazi aweze kumshauri vitu vizuri vya kufanya kwa sababu kuna vitu ambavyo mtoto anapaswa kumwambia baba yake au mama yeke, sasa unakuta mtoto anakuwa na urafiki na mtoto mwezake ambaye hawezi kumshauri vitu vizuri'' Mabeste alikiiambia kipindi cha Bomba Base Show cha redio Bomba FM Mbeya.

Mabeste ameongeza kuwa ''Kila mtu anaishi na watu kwa hiyo ili maisha yaende lazima uwe unazungumza pale endapo mwenzako anakuwa anakukwanza kwa namna moja ama nyingine, na hii pia Generation inayokuwa kwa sasa ambayo itakuwa tegemezi inapaswa kupata ukweli wa kila jambo. Kuna situation moja ipo Afrika watu hawaambiwi ukweli juu ya njia za kuepukana na Ugonjwa wa UKIMWI tayari unakuta kizazi cha sasa vishawishi vingi vimesha watawala na kuteketea na ugonjwa huo kwa hiyo elimu inapaswa kutolewa wakati kizazi hicho kikikua ili kuwa na ufahamu wa kuepukana na ugonjwa huo''

Rapper Mabeste ambaye ni Baba wa mtoto aitwaye Kendrick amewaasa wazazi kuanza sasa kujenga urafiki wenye tija kwa watoto ''Mtoto aongee na Baba, Baba aongee na Mtoto, Mwalimu aongee na Mwanafunzi, mwanafunzi aongee na Mwalimu lakini kuwe na communication yenye mipaka ya heshima lakini kuwa na urafiki baina ya mkubwa na mdogo katika kuelimisha na malezi yenye maadili''.
 
Top