Menu
 Ukimya wa miaka miwili wa Nuru The Light ulikuwa na makusudi mahsusi ya kutaka kubadilisha upepo wa muziki wa Tanzania. Ameutumia kutengeneza muziki tofauti, mzuri na utakaokuwa na ladha inayoishi kwa miaka mingi zaidi kwenye masikio ya wapenzi wa muziki.

Na sasa anarejea kwa kishindo kwa kuachia wimbo anaouelezea kama wenye utofauti mkubwa na muziki uliopo kwenye mzunguko wa nyimbo zinazochezwa kwenye redio.

Nuru anasema hakutaka ujio wake kutoka kwenye ukimya wa miaka miwili uwe wa kawaida na ndio maana ametumia muda mrefu kutengeneza kazi yake mpya aliyoipa jina ‘L’.

“Hii kazi nimeanza kuifanya tangu January,” anasema Nuru. “Ni nyimbo ambayo nimeirekodi sana. Nimefanya nyimbo nyingi lakini zaidi ni nyimbo mbili ambazo nilitaka uwe ujio wangu mpya.”

Anasema wimbo ‘L’ ndio ulioonekana kupenya zaidi na kuwa na sifa zote za kutimiza azma yake ya kurejea kwa mshindo mkuu. “Huu ni ujio mpya, kitu tofauti ambacho mimi kama Nuru nimewahi kufanya,” amesisitiza muimbaji huyo.

“Nadhani nilitaka kufanya kitu ambacho watu watasema ‘ohh kaja kitofauti tena kama vile nilivyokuja na Muhogo Andazi.”

Muimbaji huyo anaeleza kuwa L ni herufi iliyo na mambo mengi chanya na ya furaha kwenye maisha yake na ameitumia kama jina la wimbo kuyawakilisha.

“L inaweza kuwa Love, Life, Light, ni vitu chanya,” anaeleza.
Nuru amedai L ni wimbo uliotayarishwa nchini Sweden lakini aliamua kuja kuifanyia video nyumbani chini ya muongozaji mkongwe wa video, Adam.

Hii inakuwa ni video yake takriban ya tano kuwahi kufanya na muongozaji huyo.

“Nakumbuka kabisa video yangu ya kwanza Walimwengu ilikuwa ni mimi na Adam, tukasafiri tukaenda Zanzibar na nadhani tulielewa kutoka kwenye siku hiyo na ikawa imekuwa rahisi kwangu kufanya kazi naye.”

Nuru amedai kinachompa faraja zaidi ni kuwa pamoja na kutokuwa na kazi mpya kwa kipindi cha miaka miwili, bado mashabiki wamekuwa wakiwasiliana naye kumuulizia kuhusu kazi mpya.

“Nina furaha kwamba mashabiki wamekuwa wakisubiri na sasa muda umefika wa wao kuweza kusikiliza wimbo mpya.”

Usikilize wimbo huo wa mapenzi na wenye mahadhi ya ‘reggae tamu’ ambao bila shaka unajibu la swali la kwanini anasema huu ni ujio mpya.
 
Top