Menu
 

Mkuu wa Wilaya ya Kalonga, Nchini Malawi Rosemary Kalonga na Mkuu wa Wilaya ya Kyela Dk Thea Ntara.


Na Ezekiel Kamanga.
Watu 17 wakazi wa Kijiji cha Lusungo Kata ya Lusungo Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya wamekamatwa kwa kutokuwa na vyoo na uchafu wa mazingira hivyo kuzorotesha juhudi za kupambana na ugonjwa wa kipindupindu Wilayani humo.


Ugonjwa huo umedumu kwa kipindi cha miezi mitatu sasa na Kata ya Lusungo na Ndobo ndizo pekee bado zina wagonjwa wa kipindupindu hali iliyomfanya Mkuu wa Wilaya ya Kyela Dakta Thea Ntara kupiga kambi Kata ya Lusungo ili kufanya ukaguzi wa vyoo na usafi wa mazingira.


Hata hivyo juhudi za Mkuu wa Wilaya zinakwamishwa na Diwani wa Kata ya Lusungo Veronica Kanyanyila na Mwenyekiti wa Kijiji Zawadi Lugano Mwangojola ambao wamekuwa wakidai ugonjwa huo umesababishwa na imani za kishirikina na si uchafu au ukosefu wa vyoo.


Katika oparesheni hiyo maalumu iliyofanywa na Mkuu wa Wilaya aliyeambatana na Maafisa wa Afya pia iliyakumba maeneo mbalimbali kama Kata ya Ikama na Kijiji cha Tenende ambapo alilazimika kuvunja Kilabu cha pombe Kata ya Ikama baada ya kuwakuta wakazi wa eneo hilo wakinywa pombe za kienyeji katika mazingira machafu.


Mbali ya ukaguzi huo pia Mkuu wa Wilaya alishuhudia baadhi ya wananchi wakinywa pombe ya moshi na pombe zilizopigwa marufuku kutoka nchi jirani na kulazimika kuwakamata wahusika ambao wamefikishwa kituo kikuu cha Polisi Wilaya ambapo pindi uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.


Dakta Thea aliteketeza sindano zinazodhaniwa kutumika kwa ajili ya kujidunga wakati wa matumizi ya madawa ya kulevya katika Kata ya Ikama na ametoa agizo la kuwasaka wauzaji wa madawa hayo na wanaouza pombe zilizopigwa marufuku kutoka nchi jirani.


Kwa upande wake Afisa Afya Geophrey Baroshi amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu na watahakikisha kila kaya ina choo na kuwa na mazingira safi kwa muda wote ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huo Wilayani Kyela na kwamba waliokamatwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.


Mtendaji wa Kijiji cha Lusungo Fadhili Sade amesema kuwa wamefanya ukaguzi katika kaya 681 za kijiji hicho na zote hazina vyoo hali inayofanya mapambano ya kipindupindu kuwa magumu mno kwani wengi wao wamekuwa wakiamini ugonjwa huo unatokana na ushirikina.


Aidha Mtendaji wa Kata ya Lusungo Stephen John amesema wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa Diwani wa Kata na Mwenyekiti wa kijiji kuwa aache kutangaza kuwa Kata hiyo inakabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu kwani ndiyo kunachochea kuongezeka kwa ugonjwa huo ambao unatokana na ushikina na si uchafu au ukosefu wa vyoo.
 
Top