Menu
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli ametoa sababu za kumuongezea siku nne zaidi aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange. Alisema kuwa alikuwa nje ya nchi na hakuwa na mtu anayemwamini kumwachia nafasi hiyo.

Rais Magufuli aliyasema hayo Jumatatu hii wakati wa kumwapisha mkuu mpya wa majeshi, Jenerali Venance Mabeyo Ikulu jijini Dar es Salaam. Rais Magufuli alisema alipata wakati mgumu kuteua mrithi wa Jenerali Mwamunyange ndani ya siku nne. 

“Mwamunyange alistaafu rasmi Januari 31, 2017 na alinitaarifu wakati nikijiandaa kusafiri kwenda Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika (AU),” alieleza.

“Nilipokuwa nikienda kwenye mkutano wa AU, Jenerali Mwamunyange aliniambia ‘unajua siku zangu zinaisha tarehe 31 (Januari), sasa ninafanyaje, naomba umteue anayekuja.’ Nikasema ‘sasa nikiondoka leo nikamteua (mkuu mpya) tarehe 24 (Januari) na wewe unaondoka tarehe 31 (Januari), si wataanza kusema nimekutumbua?’ Kwa sababu Watanzania wanajua kubadilisha maneno kweli. 

Wataanza kusema fulani ametumbuliwa kabla ya wakati wake na hiyo ndiyo itakuwa stori,” alisema Rais Magufuli huku waliohudhuria katika hafla hiyo wakicheka.

Aliongeza, “Lakini nikamwambia ‘mimi nasafiri, ninayekujua ni wewe, ninayemteua simjui. Sasa nikishamteua ambaye simjui, hizi siku nne ambazo nitakaa nje itakuwaje?” Alihoji huku akisema kuwa ilibidi amuombe Jenerali MwamUnyange aendelee na cheo hicho mpaka atakaporudi.

Rais Magufuli alimpongeza Jenerali Devis Mwamnyange kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kipindi alipolitumikia taifa, huku akimwombea baraka kwa Mungu.
Na Emmy Mwaipopo
 
Top