Menu
 

 
Maisha ya shule yana mapito mengi. Kubwa katika yote ni kupevuka ufahamu. 
 
Ni ukweli usiopingika kuwa, kadiri mwanafunzi anavyozidi kujifunza uwezo wake wa kufikiri unakua na hivyo kumpa changamoto pana zaidi za kukabiliana na maisha.

Unapozungumzia vikwazo vya kimasomo lazima mchanganuo wa umri na ngazi za madarasa uzingatiwe ili mantiki niliyosema iwe na maana.   
 
Upo utofauti kati ya vikwazo vya mwanafunzi wa chekechea na yule wa shule ya msingi, sekondari au chuo.
 
Msingi; ni ukubwa wa ufahamu. Mahali ambapo mtoto wa shule ya awali asipoweza kutambua tatizo la fedha ya matumizi shuleni, ulinganifu hauko hivyo kwa mwanafunzi wa chuo ambaye anatakiwa kujitegemea kwa kila kitu.
 
Kama nilivyosema, kadiri unavyoelimika, unauongezea ubongo kazi ya uchambuzi. Ukubwa wa ufahamu utakufanya uwe mdadisi wa kila kitu na hivyo kujiweka katika hatari ya kupata msongo wa mawazo.
 
Wanasaikolojia wameshindwa mara nyingi kuuzungumzia msongo wa mawazo mazuri kwa sababu hauna hasara za moja kwa moja, badala yake wametazama zaidi msongo wa mawazo yanayoumiza ambao hushambulia vichocheo vya uelewa na hivyo kumfanya mtu ashindwe kupata msaada wa fikra kutoka kwenye akili yake.
 
Uchunguzi unaonesha kuwa, wanafunzi wengi wameshindwa kufanya vizuri kimasomo kutokana na tatizo kuu la msongo wa mawazo yanayoumiza. 
 
Mfano kuachwa kimapenzi, kusalitiwa, kufiwa na walezi au wazazi, kukabiliana hali ngumu ya kimaisha au kukosa msaada juu ya matatizo fulani.
 
Mwanafunzi yeyote hata mwenye akili ya miujiza akiruhusu msongo wa mawazo hawezi kufaulu mitihani, hawezi kufanya vizuri kimasomo, atajikuta anaporomoka na kuishia pabaya.
 
Pengine kutokana na nafasi niliyonayo kwenye safu hii, nijibu swali mwanafunzi afanye nini kukabiliana na kikwazo hiki cha msongo wa mawazo?.
 
Kwanza, ni kukubali kupokea tatizo. Watu wengi wanaumizwa na mawazo kwa sababu wanadhani hawastahili kupata tatizo husika. 
 
Changamoto yoyote inayokupata ipokee kwanza halafu itafutie ufumbuzi kwa kuwashirikisha watalaamu wa masuala ya saikolojia, rafiki au ndugu wenye uelewa wa kutosha, huku wewe mwenyewe ukipuuza ukubwa wa tatizo.

Post a Comment

 
Top