Menu
 

WATU wengi wamekuwa wepesi sana kukimbilia kwa rafiki zao ili kuomba msaada wa mawazo ya nini wafanye  kwenye maisha na hasa wakati wa shida.

 Imani iliyojengeka kwa wengi katika jamii yetu ni kuwa, ushauri ni kitu muhimu sana kwa kila hatua.

Kwa mtazamo wa harakaharaka unaweza kuishia kwenye ukomo huo wa fikra na kuamini juu ya ushauri wa mtu kukufikisha mahali sahihi kwenye maisha. Unapokwama kimaisha unakimbilia kushauriwa, wakati mwingine hata unapotaka kuoa au kuachana na umpendaye, unamuomba rafiki yako ushauri.

Je, umeshawahi kufikiria hasara za kuomba ushauri wa kimaisha kwa rafiki yako? Hebu ungana nami nikumegee kidogo hasara za ushauri.

UTAKUPOTOSHA
Ni wazi kwamba kipimo cha uelewa kinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Ifahamike kuwa, uhodari wa mambo nao hutofautiana, mtu anaweza kuwa mahiri katika siasa na akaaminika kwenye jamii, lakini ukimpelekea suala la mapenzi anakuwa hajui kitu, hivyo ni rahisi kukupotosha.

 Uchunguzi unaonyesha kuwa, watu wengi sana hupotoshwa na rafiki zao wasiokuwa na uelewa wa kutosha juu ya tatizo au suala husika la kimaisha. Ushauri wangu ni kuwa makini kila unaposhauriwa.


UTARAHISISHA MAMBO
Mara nyingi washauri huwa si wao wanaokabiliana na mambo, hivyo ni rahisi kwao kupima vitu kwa juujuu tu na kushauri kirahisirahisi.
Ni rahisi kumsikia mshauri akisema: “Vipi kakupiga namna hii, aaa huyu si mwanaume kwa kweli ni bora ukaachana naye.”
Anasema ni bora kuachana naye kwa sababu haumizwi na kuachana, unayeachana ni wewe anayekushauri.

“Tatizo hili ni dogo sana, kama hataki kukulipa mpeleke mahakamani.” Kwa mshauri ni rahisi kusema hivyo lakini kumbuka ukubwa wa usumbufu wa kwenda mahakamani kupoteza muda litakuwa ni suala lako si lake tena. Uwe makini na ushauri unaorahisisha mambo.

UTAKUGEUZA
Ulimwenguni kuna watu wa kila namna wenye mapenzi na mguso tofauti wa kimaisha, hii inamaana kwamba mtu fulani hawezi kulingana na mwingine kwa kila kitu; ni nadra sana.
Uzoefu unaonyesha kuwa, washauri wengi hushauri kwa uzoefu wao na mapenzi yao, lakini je ni sahihi uzoefu na  mtazamo wao uwe msaada kwa watu wengine?

Jibu ni hapana, kinachotokea mara nyingi kwenye ushauri ni mtu kumfanya mwenzake awe kama yeye alivyo, yaani apuuze, aamue na apende kama staili yake, jambo ambalo haliwezekani kabisa. Vipi Juma ageuke ghafla awe kama Hassan kwenye suala la mapenzi? Ushauri ni muhimu lakini upime kama unalingana na matakwa yako.

 UTAKUONDOLEA UJASIRI
“Kwa maelezo hayo mumeo ni malaya sana, naona itakuwa vigumu kumbadilisha, ni bora ukaanza maisha yako kwa sababu kuna siku hali itakuwa mbaya.”
Huu ni ushauri ambao unaweza kumuondolea mtu ujasiri wa kukabiliana na tabia ya mumewe hadi kufikia hatua ya kumsaidia akaachana na tabia zake mbaya.

Ushauri huondoa ujasiri wa kukabili tatizo hasa pale anayekushauri atakapolipeleka suala lako kwenye njia ngumu isiyokuwa na ufumbuzi. Ikumbukwe kuwa anayeamini kushindwa ni mshauri lakini wewe kama binadamu mwenye uwezo mkubwa unaweza kusimama kutetea penzi lako na kuliweka sawa mpaka jamii ikasema: “Jamani huyu dada kamrekebisha kweli mumewe, hakuwa hivi alikuwa mlevi lakini sasa kaacha pombe.”

UTAKUNYIMA FURSA
Kwenye maisha kuna fursa nyingi za mafanikio ambazo unaweza usizipate ukiwa mtu wa kusikiliza sana ushauri wa watu. Kuna wakati ambao unatakiwa usimame wewe kuamua ufanye nini hata kama jamii na washauri watakuona kama unakosea. Akili za kuambiwa changanya na zako, wanasema waswahili. 
Credit:- Rich Manyota.

Post a Comment

 
Top