Menu
 


Mabingwa wa soka Afrika mashariki na kati Azam FC wametangaza kuhamishia nguvu zao katika mshike mshike wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, baada ya kuondolewa kwenye michuano ya kombe la shirikisho hatua ya robo fainali.


Azam FC waliondoshwa kwenye michuano hiyo siku ya jumamosi baada ya kukubali kufungwa kwa penati tisa kwa nane na Mtibwa Sugar ambao sasa wameingia hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho.


Afisa habari wa Azam FC Jaffari Iddy Maganga amesema tayari kikosi chao kimeshaanza maandalizi ya mchezo ujao wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City ambao utachezwa jijini Mbeya.


Katika hatua nyingine Jaffari Iddy Maganga amesema hali ya beki wao David Mwantika ambaye alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar na kulazimika kukimbizwa hospitali, inaendelea vizuri na hii leo walikua wakitarajia taarifa za mwisho kutoka kwa madaktari wa hospitali ya taifa ya Muhimbili.


Mwantika alipata tatizo hilo dakika ya 64 na kupatiwa matibabu ya awali kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mbagala Zakhem na kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke, na baadaye ile ya Rufaa ya Muhimbili (MNH).

Post a Comment

 
Top